Rais Rouhani asisitiza mapambano ya kurejesha haki za Wapalestina kutoka kwa Wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i21385-rais_rouhani_asisitiza_mapambano_ya_kurejesha_haki_za_wapalestina_kutoka_kwa_wazayuni
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema leo hii maudhui ya Palestina na ukombozi wa Quds Tukufu ni takwa la Waislamu wote duniani.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Dec 14, 2016 00:56 UTC
  • Rais Rouhani asisitiza mapambano ya kurejesha haki za Wapalestina kutoka kwa Wazayuni

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema leo hii maudhui ya Palestina na ukombozi wa Quds Tukufu ni takwa la Waislamu wote duniani.

Rais Rouhani ameyasema hayo Jumanne mjini Tehran wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Ramadhan Abdullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul- Islami ya Palestina na kuongeza kuwa, kadhia ya ukombozi wa Quds Tukufu na taifa la Palestina kupata haki zake zote inapaswa kuwa kadhia muhimu zaidi katika eneo.

Rais wa Iran amesema njama mbali mbali zisiwe kizingiti katika njia ya taifa la Palestina kufikia malengo yake na kuongeza kuwa, makundi yote ya kupigania ukombozi wa Palestina yana jukumu muhimu kuhusu suala hili.

Rais Rouhani amesema kuwa, tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeendelea kuunga mkono mapambano ya taifa la Palestina.

Rais wa Iran amesema leo waliowengi duniani wanakubali kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel haujawahi kufuatilia amani na kwa msingi huo suala hilo linapaswa kutumiwa kuonyesha kuwa Wapalestina hawana njia nyingine isipokuwa Jihadi na Muqawama au mapambano kwa ajili ya kukabiliana na utawala huo ghasibu.

Wapiganaji wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina

Rais Rouhani ameashiria ushindi wa hivi karibuni wa wananchi wa mataifa ya eneo dhidi ya magaidi wanaopata misaada na uungaji mkono wa utawala wa Kizayuni na kusema, kwa yakini kupitia mapambano, kujitolea muhanga, kusimama kidete, umoja na kuunganisha pamoja nguvu za Ulimwengu wa Kiislamu wananchi wa mataifa ya eneo wanaweza kupata ushindi na kufeli njama zote za kupotosha fikra za umma kuhusu maudhui ya Palestina.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uungaji mkono wake kwa taifa linalodhulumiwa la Palestina. Ramadhan Abdullah amesisitiza kuwa, pamoja na kuwepo mashinikizo, Wapalestina wangali wanaendeleza mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni. Amesema mapambano hayo yataendelea hadi pale utawala ghasibu wa Israel utakapoondolewa kikamilifu katika ardhi za Palestina.