Rais Rouhani awasili Bishkek baada ya kukamilisha safari yake Kazakhstan
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alasiri ya leo amewasili katika mji mkuu wa Kyrgyzstan, Bishkek baada ya kukamilisha ziara yake katika nchi jirani ya Kazakhstan.
Inatarajiwa kuwa Rais Rouhani ambaye yuko katika safari ya kuzitembelea nchi kadhaa za Asia ya Kati atakutana na kubadilishana mawazo na mwenyeji wake wa Kyrgyzstan, Almazbek Atambayev.
Kabla ya kuelekea Kyrgyzstan, Rais Rouhani alikuwa nchini Kazakhstan akiongoza ujumbe wa maafisa wa ngazi za juu wa Iran. Amesema katika kikao cha kamisheni ya pamoja mjini Astana kwamba nchi hizo mbili zimepiga hatua muhimu katika njia ya ustawi na kuimarisha uhusiano wa pande mbili na kwamba mwenendo huo unapaswa kudumishwa kwa kusahilisha mahusiano ya kibiashara na ushirikiano wa kibenki na masuala ya visa.
Rais Rouhani pia ameipongeza Kazakhstan kutokana na mchango wake mzuri wakati wa mazungumzo ya nyuklia kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kundi la 5+1 na kusema: Nchi mbili za Iran na Kazakhstan daima zimekuwa marafiki na zinazosaidiana katika jumuiya za kimataifa. Amesisitiza kuwa ushirikiano huo unapaswa kuimarishwa zaidi.
Kwa upande wake Rais Nursultan Nazarbayev wa Kazakhstan amesema Iran ni nchi muhimu na rafiki wa Kazakhstan katika ulimwengu wa Kiislamu na kwamba siasa na misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu imekuwa na taathira chanya kikanda na kimataifa.
Mwishoni mwa safari ya Rais Hassan Rouhani nchini Kazakhstan, pande hizo mbili zimetia saini hati 5 za maelewano katika masuala mbalimabli ya ushirikiano wa kibiashara, kibenki, usafirishaji wa baharini na kadhalika.