Iran na Ufaransa katika ukingo wa kufunguliwa ukurasa mpya wa ushirikiano
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo amekamilisha safari yake nchini Italia na kuelekea Ufaransa baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis.
Safari ya Rais Rouhani nchini Ufaransa ni ya pili barani Ulaya baada ya kuanza kutekelezwa makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Akiwa nchini Ufaransa Rais Rouhani amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo. Hata kama mazungumzo ya sasa ya Iran na Ulaya yamejikita zaidi katika kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika uga wa kiuchumi baada ya taifa hili kuondolewa vikwazo, lakini umuhimu wa safari ya Rais Rouhani barani Ulaya unapaswa kutathminiwa katika masuala ya zaidi ya uhusiano wa kiuchumi. Hii ni kutokana na kuwa, katika hali ya sasa kumeandaliwa mazingira mwafaka zaidi baada ya makubaliano ya nyuklia ya Iran na kundi la 5+1 kwa ajili ya kupanua zaidi ushirikiano kati ya Iran na Ulaya. Wiki iliyopita pia, Rais Xi Jinping wa China alifanya safari hapa mjini Tehran na kufanya mazungumzo muhimu na viongozi wa ngazi za juu wa Iran katika uwanja wa kiuchumi na kisiasa kati ya Tehran na Beijing. Filihali, dira mwafaka ya ushirikiano imeelekezwa barani Ulaya, jambo ambalo linaonesha juu ya kuweko uwiano katika ushirikiano wa Iran na Ulaya na Asia. Ukweli wa mambo ni kuwa, safari hizi zinaweza kusaidia kudiriki kwa uhalisia wake masuala mbalimbali, migogoro pamoja na fursa za ushirikiano wa pande kadhaa. Katika safari yake hapo kabla hapa mjini Tehran, Gerard Larcher, Spika wa Baraza la Seneti la Ufaransa aliitaja Iran kuwa nchi yenye uthabiti katika Mashariki ya Kati na kwamba, taifa hili limekuwa na tajiriba mwafaka katika kulinda amani na usalama.
Safari ya ujumbe wa ngazi za juu wa kiuchumi na kisiasa wa Ufaransa nchini Iran baada ya kufikiwa makubaliano ya nyuklia, nayo inaweza kutathminiwa kuwa ni kuanza msimu mpya wa kuleta harakati kwa ajili ya ustawi na ushirikiano baina ya nchi mbili hizi. Kwa sasa mwenendo huo unaonekana kuchukua kasi zaidi. Iran nayo inaitambua Ufaransa kama nchi muhimu barani Ulaya na katika kumbukumbu zake ina fikra chanya kuhusu Ufaransa katika zama za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Kuishi uhamishoni Imam Khomeini huko Neauphle-le-Château ni jambo ambalo limelifanya jina la Ufaransa libakie kwenye kumbukumbu na fikra za wananchi wa Iran wanaoitambua Ufaransa kama nchi yenye watu watamaduni. Hivi sasa udharura wa kustawisha uhusiano kati ya Iran na nchi za Ulaya unahisika zaidi kuliko huko nyuma. Uhusiano huo unaweza kujumuisha nyuga za kupambana na ugaidi, vitendo vya utumiaji mabavu na misimamo ya kufurutu ada ambayo Ufaransa yenyewe imepata pigo katika masuala hayo na hivyo kuwa sababu ya kukuzwa zaidi uhusiano kati ya Tehran na Paris. Makubaliano ya nyuklia yamethibitisha kwamba, masuala muhimu ya kimataifa yanaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kutumia mazungumzo na njia za kimantiki. Matukio ya kigaidi ya mwaka mmoja uliopita nchini Ufaransa na katika maeneo mengine ya dunia yameonesha kuwa, ugaidi ni tishio na hatari kubwa kwa nchi na mataifa yote duniani. Hapana shaka kuwa, utatuzi wa masuala kama ya ugaidi, mgogoro wa Syria na suala la wahajiri ni mambo ambayo yanahitajia ushirikiano na uelewa wa pamoja. Katika uwanja huu, Iran na Ufaransa nazo zinaweza kuwa na ushirikiano na ushiriki mzuri. Huko nyuma pia nchi mbili hizi zimewahi kuwa na ushirikiano katika masuala mbalimbali; na hii leo kumejitokeza mazingira muhimu zaidi ili pande hizo mbili ziweze kustafidi na anga hii nzuri iliyojitokeza.