Iran yakanusha madai ya kukataa kutuma mahujaji mwaka huu
(last modified Wed, 04 Jan 2017 16:21:35 GMT )
Jan 04, 2017 16:21 UTC
  • Iran yakanusha madai ya kukataa kutuma mahujaji mwaka huu

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekanusha madai yanayosema kuwa, Tehran imekataa kutuma mahujaji wake mwaka huu na kusema kuwa madai hayo hayana ukweli wowote.

Bahram Qasemi amesema, kama ilivyotangazwa huko nyuma, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hadi hivi sasa haijapokea barua yoyote kutoka kwa Saudi Arabia.

Amesema: Kwa mara nyingine tunapenda kusisitiza kwamba, ni jambo lililo wazi kuwa, kama mwaliko huo utatolewa na mazingira yakawa yanaruhusu, basi suala la kutumwa mahujaji litashughulikiwa na taasisi husika na vyombo hivyo ndivyo vitakavyochukua maamuzi.

Kabla ya hapo kulikuwa na taarifa kuwa, Wizara ya Hija ya Saudi Arabia imezitumia barua nchi 80 duniani ikiwemo Iran kuzialika kushiriki katika mjadala wa kufanikisha ibada ya Hija mwaka huu.

Maelfu ya Waislamu waliuawa kwenye maafa ya Mina na Saudi Arabia inakasirika kila inapolaumiwa kwa uzembe uliofanyika kwenye tukio hilo chungu.

Hata hivyo Taasisi ya Hija na Ziara ya Iran imesema, haijapokea barua yoyote kutoka kwa Wizara ya Hija ya Saudi Arabia.

Itakumbukwa kuwa, mwezi Septemba 2015, maelfu ya Mahujaji walipoteza maisha yao katika mazingira mabaya sana kwenye eneo la Mina nchini Saudia Arabia, kutokana na usimamiaji mbovu wa ibada hiyo.

Iran ilisimama kidete kulalamikia uzembe huo, jambo ambalo liliwakasirisha viongozi wa Saudia na kuwafanya waweke masharti magumu sana yaliyowanyima Waislamu wa Iran haki yao ya kutekeleza ibada ya Hija mwaka jana.

Tags