Iran: Utawala wa Kizayuni hauna nafasi yoyote Mashariki ya Kati
-
Alauddin Boroujerdi, Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran)
Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel hauwezi kuwa na nafasi yoyote katika eneo la Mashariki ya Kati iwapo Waislamu watashikamana na kuwa kitu kimoja.
Alauddin Boroujerdi amesema hayo mjini Beirut wakati alipoonana na wawakilishi wa makundi mbalimbali ya Palestina yaliyoko nchini Lebanon na kuongeza kuwa, ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba kwa kukombolewa ardhi zote za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel, utawala wa Kizayuni hautakuwa na nafasi yoyote katika jiografia ya kisiasa ya eneo la Mashariki ya Kati.
Amegusia miongozo ya Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyesimama imara kuunga mkono na kusaidia malengo matukufu ya Palestina hadi zitakapokombolewa ardhi zote za taifa hilo na kuongeza kuwa, misimamo ya Iran daima imekuwa ni kuunga mkono malengo matukufu ya Palestina na inaamini kuwa jambo hilo haliwezi kufanikiwa ila kwa kuweko umoja na mshikamano baina ya Waislamu.
Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya Bunge la Iran aidha amesema, maadui wa Uislamu wanafanya njama za kushadidisha mizozo katika safu za Waislamu hivyo ni wajibu wa mataifa yote ya Waislamu kuzijua vyema njama hizo na kuungana pamoja katika kadhia ya Palestina na kulinda malengo matukufu ya taifa hilo madhlumu.
Aidha Boroujerdi amezilaumu baadhi ya nchi za Waislamu za eneo hili kama vile Bahrain kwa kuwa na uhusiano na utawala wa Kizayuni na kusisitizia wajibu wa Waislamu kuwa macho. Ujumbe wa Bunge la Iran unaoongozwa na Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya bunge hilo uliingia nchini Lebanon siku ya Alkhamisi kwa kutumia mpaka wa nchi kavu wa Syria.