Rouhani: Iran iko tayari kuimarisha uhusiano wake na Albania
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema kipindi hiki cha baada ya vikwazo vya kidhalimu dhidi ya taifa hili sambamba na kutekelezwa makubaliano ya nyuklia ya Vienna ni mwafaka kwa kuimarisha uhusiano wa pande mbili wa Jamhuri ya Kiislamu na Albania.
Katika mazungumzo yake na Ditmir Bushati, Waziri wa Mambo ya Nje wa Albania hapa mjini Tehran, Rais Rouhani amesema kipindi hiki cha kuondolewa vikwazo Iran ni fursa nzuri ya kuimarishwa uhusiano na ushirikiano kati ya Tehran naTirana katika nyuga mbalimbali, hususan ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara. Amebainisha kuwa, Iran na Albania zina historia ya jadi na tamaduni zinazofanana huku akipongeza ushirikiano wa nchi mbili hizi katika nyuga za elimu na sayansi.
Kiongozi wa taifa la Iran amesisitiza kuwa, sekta binafsi za Jamhuri ya Kiislamu na Albania zinaweza kutumia fursa hii kuboresha zaidi mahusiano yao.
Kadhalika Rais Hassan Rouhani wa Iran amesisitizia udharura wa kuimarishwa vita dhidi ya ugaidi, misimamo ya kufurutu ada na ghasia katika pembe mbalimbali za dunia.
Wakati huohuo, Dakta Hassan Rouhani wa Iran ameishukuru serikali ya Tirana kwa kutuma salamu za rambirambi kwa serikali na taifa la Iran, kufuatia kifo cha Ayatullah Hashemi Rafsanjani, aliyekuwa Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran.
Kwa upande wake, Ditmir Bushati, Waziri wa Mambo ya Nje wa Albania amesema kuwa, nchi yake iko tayari kufungua ukurasa mpya wa mahusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kila uga.
Amefafanua kuwa, utekelezwaji wa makubaliano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) umefungua ukurasa mpya wa Albania kuboresha uhusiano wa pande mbili na Tehran katika nyuga za maendeleo na uchumi.