Jan 16, 2017 07:32 UTC
  • Rais Rouhani: Ayatullah Rafsanjani alikuwa msaidizi imara wa Kiongozi Muadhamu

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Kuaga dunia Ayatullah Hashemi Rafsanjani aliyekuwa Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran, ni msiba mkubwa ambao umepelekea Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kupoteza tegemeo lake kubwa."

Rais Rouhani aliyasema hayo Jumapili mjini Tehran katika kikao cha baraza la mawaziri na kuongeza kuwa, Ayatullah Rafsanjani alikuwa msaidizi imara wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Aidha amesema huduma za Ayatullah Rafsanjani kwa Uislamu, Mapinduzi ya Kiislamu na taifa la Iran ni sababu ya kimsingi iliyopelekea idadi kubwa ya watu kujitokeza katika mazishi yake.

Hassan Rouhani aidha ametoa wito kwa  maafisa wa serikali na wale wote waliompenda marehemu Ayatullah Hashemi Rafsanjani kujitahidi zaidi kuwahudumiwa wananchi sambamba na kumuunga mkono Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Ayatullah Rafsanjani aliaga dunia Jumapili iliyopita   baada ya umri mrefu wa jihadi na jitihada zisizo na kikomo kwa ajili ya Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu.

Khitma ya marehemu Ayatullah Hashemi Rafsanjani

Ayatullah Rafsanjani, ambaye aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 82 kutokana na mshtuko wa moyo,  alizikwa Jumanne katika Haram Takatifu ya Imam Khomeini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Wakati huo huo khitma ya siku ya saba ya marehemu Ayatullah Hashemi Rafsanajani imefanyika katika Haram Takatifu ya Imam Khomeini MA na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya watu wa matabaka mbali mbali.

Tags