Rais Rouhani: Iran ni nchi ya amani na ya kirafiki
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu daima katika kipindi chote cha histroia yake imekuwa ni yenye kufuatilia suala la kuweko amani na urafiki.
Rais Rouhani amesema hayo leo hapa mjini Tehran katika hotuba yake kwenye mkutano wa 17 wa utalii unaojulikana kama "World Federation of Tourist Guide Associations Convention" na kubainisha kwamba, nchini Iran kuna maisha ya amani baina ya wafuasi wa dini za Mwenyezi Mungu kando ya msikiti na kanisa na kwamba katika Bunge la Iran wafuasi wa dini za Uyahudi, Ukristo na Uzartoshti wana wawakilishi wao wakiwa pamoja na wawakilishi wa Waislamu katika Bunge hilo.
Rais wa Iran amesema, moja ya malengo makuu ya taifa lenye utamaduni na ustaarabu wa miaka elfu saba wa Iran katika Mashariki ya Kati na ulimwengu kwa ujumal ni kuweko mfungamano baina ya mataifa mbalimbali.
Rais Rouhani amesema kuwa, hizi si zama za mataifa kujengeana ukuta na kwamba hata kama kutakuweko ukuta baina ya mataifa, basi ukuta huo unapaswa kuvunjwa na hivyo kuondoa vizuizi baina ya mataifa.
Rais Hassan Rouhani sambamba na kutangaza utayari wa Iran wa kusaidia kupambana na ugaidi katika eneo lolote lile duniani amesema kuwa, kwa bahati nzuri hii leo ugaidi unaelekea kutokomea katika Mashariki ya Kati.