Morocco yasema haitaitambua Sahara Magharibi licha ya kurejea AU
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i24757-morocco_yasema_haitaitambua_sahara_magharibi_licha_ya_kurejea_au
Serikali ya Rabat imesema katu haitatambua uhuru wa Jamhuri ya Sahara Magharibi licha ya Morocco kukubaliwa kurejea katika Umoja wa Afrika AU baada ya kuondoka zaidi ya miongo mitatu iliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 06, 2017 04:10 UTC
  • Morocco yasema haitaitambua Sahara Magharibi licha ya kurejea AU

Serikali ya Rabat imesema katu haitatambua uhuru wa Jamhuri ya Sahara Magharibi licha ya Morocco kukubaliwa kurejea katika Umoja wa Afrika AU baada ya kuondoka zaidi ya miongo mitatu iliyopita.

Nasser Bourita, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco amesema kuwa, mbali na nchi hiyo kutoitambua Sahara Magharibi, lakini pia itafanya juhudi na kuanzisha lobi za kuzishawishi nchi za Kiafrika zinazolitambua eneo hilo kuwa jamhuri huru, kubadili mtazamo na msimamo wao.

Wiki iliyopita katika mkutano wa Umoja wa Afrika huko Addis Ababa, Ethiopia, AU ilikubali tena uanachama wa Morocco, miaka 33 baada ya kujiondoa umoja huo, kutokana na mgogoro wa Sahara Magharibi ambao hadi sasa haujatatuliwa.

Viongozi wa Afrika walipokutana Addis Ababa wiki jana

Mwaka 1984 Morocco ilijiondoa katika Umoja wa Afrika AU, wakati huo ukijulikana kama OAU, baada ya eneo la Sahara Magharibi kukubaliwa kama mwanachama wa umoja huo. Morocco ilichukua udhibiti wa Sahara Magharibi kutoka mkoloni mwa Mhispania mwaka 1975  na inasisitiza kuwa eneo hilo ni sehemu ya ardhi yake. 

Hii ni katika hali ambayo, Brahim Ghali, Rais wa harakati ya Polisario inayoshinikiza kutambuliwa Jamhuri ya Kiarabu ya Sahara Magharibi kama taifa huru ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, kwa sasa machaguo yote yapo mezani; iwapo njia za kidiplomasia na mazungumzo ya amani hazitafua dafu, watalazimika kuanzisha upya makabiliano ya silaha.