Velayati: Marekani inafaa kuilipa fidia Iraq kwa kuivamia 2003
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i24765-velayati_marekani_inafaa_kuilipa_fidia_iraq_kwa_kuivamia_2003
Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kistratejia cha Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran amesema serikali ya Iraq inapaswa kupigania haki ya kufidiwa na Marekani katika vyombo vya kimataifa, kutokana na uvamizi wa utawala wa Washington dhidi yake mwaka 2003.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 06, 2017 04:34 UTC
  • Velayati: Marekani inafaa kuilipa fidia Iraq kwa kuivamia 2003

Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kistratejia cha Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran amesema serikali ya Iraq inapaswa kupigania haki ya kufidiwa na Marekani katika vyombo vya kimataifa, kutokana na uvamizi wa utawala wa Washington dhidi yake mwaka 2003.

Akiongea na waandishi wa habari akiwa pamoja na Jan Kubis, Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq hapa Tehran jana Jumapili, Dakta Velayati alisema serikali ya Washington ililisababishia maafa na hasara kubwa taifa hilo la Kiarabu, kutokana na uvamizi wake mwaka 2003, kwa kisingizio cha kutaka kumuangamiza Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Marekani inafaa kuwajibishwa na kulazimishwa kulilipa fidia taifa hilo, kwa kuua maelfu ya watu wasio na hatia na kuvuruga uchumi wa nchi kwa kusambaratisha kwa mabomu nyumba na miundombinu ya nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta.

Wanajeshi wa Marekani nchini Iraq

Kwa upande wake, Jan Kubis, Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq amesema angependa kuona uchunguzi huru na wa kina ukifanyika dhidi wakuu wa Washington waliotoa uamuzi wa kutuma vikosi vya jeshi Iraq mwaka 2003, eti kulikomboa taifa hilo kutokana na 'ugaidi wa Saddam Hussein.' 

Mara baada ya kuchaguliwa Rais Donald Trump wa Marekani alisema kuwa nchi hiyo ilifanya makosa kuzivamia nchi za Iraq na Afghanistan. Katika mahojiano yake yaliyochapishwa na gazeti la Times la Uingereza, Trump alikosoa siasa za nje za Marekani na kusema: Uvamizi wa Iraq na Afghanistan ni miongoni mwa maamuzi mabaya zaidi katika historia ya Marekani.