Jahangiri: Lugha za vitisho dhidi ya Iran zimeshindwa na hazina athari yoyote
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, tawala na watu wanaozungumza na taifa kubwa la Iran kwa lugha za vitisho ndio washindwa wakuu katika medani.
Es-haq Jahangiri, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amesisitiza kuwa, taifa la Iran katu halitishiki wala haliogopeshwi na lugha hizo za vitisho.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taifa hili linakaribisha kwa mikono miwili ushirikiano, lakini watu ambao wanazungumza na taifa hili kwa lugha za vitisho ndio washindwa halisi.
Aidha Jahangiri ameashiria matamshi ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuwapiga marukufu kuingia nchini humo raia wa Kiirani na kubainisha kuwa, Wamarekani wamechagua mbinu chafu na mbaya na kwamba, taifa la Iran lina matumaini mbinu hiyo itaachwa na kisha serikali ya Washington kuchagua njia ya ushirikiano.
Kadhalika Es-haq Jahangiri, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kwamba, baina ya Iran na serikali ya Marekani kuna ukuta mrefu wa kutoaminiana na kuongeza kuwa, mambo mengi yaliyofanywa na Marekani kuhusiana na Iran, kwa hakika katu hayawezi kufutika katika fikra za wananchi wa taifa hili.