Uhusiano wa Iran na Oman wazidi kuimarika, Rais Rouhani atembelea Muscat
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, kuna ulazima wa kuimarishwa ushirikiano wa pande zote baina ya nchi za eneo hili, kama ambavyo kuna wajibu pia wa kupewa kipaumbele suala la kusimamisha vita na kusaidiwa wananchi wa Yemen.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hayo leo mjini Muscat wakati alipoonana na Sultan Qaboos wa Oman na kusema kuwa, nchi mbili ndugu za Iran na Oman zina nafasi muhimu sana katika kulinda usalama wa eneo hili.
Rais Rouhani amesema, nchi mbili za Iran na Oman ndio walinzi wa jadi wa Lango Bahari la Hormouz ambayo ni njia yenye usalama na huru kwa ajili ya biashara za kimataifa. Amesema, ushirikiano wa Iran na Oman katika kulinda usalama, utulivu na ustawi wa eneo hili, ni muhimu sana.
Aidha Rais Rouhani amesema, kwa ajili ya kulinda usalama wa eneo hili, hakuna njia yoyote nyingine ya kimsingi kuliko kila nchi ya eneo hili kutekeleza vizuri majukumu yake na kuweko ushirikiano wa ndani ya eneo hili, usioathiriwa na mikono ya kigeni.
Hivyo nchi zote za eneo hili zinapaswa kushirikiana katika kulinda usalama na kuleta utulivu wa kudumu. Aidha amepongeza juhudi za kustawisha zaidi na zaidi uhusiano baina ya Iran na Oman na kusema, Tehran haitosita hata mara moja kuzisaidia nchi ambazo zina matatizo yakiwemo matatizo ya ugaidi.
Kwa upande wake Sultan Qaboos wa Oman amesema, Muscat inapenda kuimarisha uhusiano wake na Tehran katika nyuga zote za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.
Sultan wa Oman ameipongeza Iran kwa kuwa tayari wakati wote kustawisha uhusiano wake na majirani zake na kuimarisha ushirikiano wa kieneo.
Aidha amesema: Kuimarika uhusiano wa Iran na nchi za eneo hili ni kwa faida ya maendeleo, usalama na utulivu wa eneo hili zima.
Mara baada ya safari yake nchini Oman, Rais Hassan Rouhani ameelekea moja kwa moja nchini Kuwait ambako amepokewa rasmi na Amir wa nchi hiyo, Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah.
Akiwa nchini Kuwait, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ataonana na kufanya mazungumzo na viongozi wengine pia wa ngazi wa nchi hiyo.