Iran: Silaha za nyuklia za Israel ni tishio kwa usalama wa dunia
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, maghala ya silaha za nyukli ya utawala haramu wa Israel ni tishio kubwa zaidi kwa amani na usalama wa dunia.
Bahram Qasemi ameashiria madai yasiyo na msingi yaliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu dhidi ya miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran na kusema: Israel ina mamia ya mabomu ya nyuklia katika maghala yake na inahesabiwa kuwa tishio kubwa zaidi la usalama na amani ya Mashariki ya Kati na dunia nzima.
Qasemi ameongeza kuwa, madai hayo yasiyo na mashiko dhidi ya Iran yametolewa na utawala ambao hauheshimu hata kidogo sheria za kimataifa na faili lake limejaa jinai zisizo na hisabu na ukatili mkubwa dhidi ya watu wanaoendelea kudhulumiwa wa Palestina na nchi nyingine jirani na Palestina.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, matamshi ya Donald Trump na Benjamin Netanyahu katika mkutano wa waandishi wa habari hayana jipya isipokuwa kukariri madai yasiyo msingi wala thamani yoyote kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran.
Amesema madai hayo yanapingana na ripoti za mara kwa mara za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki zilizothibitisha kuwa miradi ya nyuklia ya Iran inafanyika kwa malengo ya amani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, kwa mujibu wa fatuwa iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi nchini Iran Ayatullah Ali Khamenei, silaha za nyuklia hazina nafasi yoyote katika sera za kijeshi za Iran.