Rouhani: Israel ni utawala pandikizi mzaliwa wa Magharibi
(last modified Wed, 22 Feb 2017 16:55:45 GMT )
Feb 22, 2017 16:55 UTC
  • Rouhani: Israel ni utawala pandikizi mzaliwa wa Magharibi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, kadhia ya Palestina ndiyo kadhia muhimu zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu na kwamba, utawala wa Kizayuni ni utawala pandikizi, mzaliwa wa Magharibi unaovunja haki za binadamu.

Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo Jumatano wakati akifunga Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina hapa mjini Tehran. 

Rais Rouhani ameashiria historia ya kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na kusisitiza kuwa, Palestina si tatizo la kaumu au taifa moja tu, bali kwa upande mmoja suala hilo linaonesha dhulma, ukandamizaji na kudharauliwa haki na sheria za kimataifa na kutokuwa na maana mashirika ya kimataifa na kwa upande mwingine ni nembo ya jitihada na jihadi za kuendelea za taifa fulani katika kupigania haki zake tena kwenye dunia hii iliyojaa dhulma, ukwamishaji wa jamii ya kimataifa na uzembe wa baadhi ya nchi za Kiislamu.

Rais Hassan Rouhani katika Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina

 

Aidha amesema, vitendo vya kichochezi na kuendelea kuporwa na kukaliwa kwa mabavu ardhi za wananchi wa Palestina sambamba na njama zenye malengo maalumu za kujaribu kubadilisha utambulisho wa kihistoria na kiustaarabu wa ardhi za Palestina ni mambo ambayo pole pole yameleta maafa kwa usalama na amani ya dunia nzima.

Amesema, Wazayuni wanajaribu kuwafanya walimwengu waamini kuwa Wapalestina ni wakimbizi ambao inabidi waishi wakihangaika huku na huko bila ya kuwa na ardhi yao kama ambavyo pia Wazayuni wanafanya njama za kuuonesha muqawama kuwa ni ugaidi.

Wananchi wa Palestina katika Intifadha ya kupambana na utawala kandamizi wa Israel

 

Rais Rouhani amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa, amani ya pande zote na ya kiuadilifu haiwezi kupatikana Mashariki ya Kati bila ya kumalizwa kwanza mgogoro wa kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na kuheshimiwa kikamilifu haki za taifa hilo ikiwemo haki ya kujiainishia mustakbali wake, kurejea nyumbani wakimbizi wote wa Palestina na kuundwa nchi moja ya Palestina ambayo mji mkuu wake ni Baytul Muqaddas kupitia kufanyika kura ya maoni itakayoyashirikisha makabila na kaumu zote zenye asili na Palestina, wawe ni Waislamu, Wakristo au Mayahudi.