Velayati: Mpango wa ulinzi wa Iran hauna uhusiano wowote na Marekani
Mkuu wa kituo cha utafiti wa kistratijia cha Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran amesema: Mfumo wa makombora wa Iran ni wa kiulinzi na wa lengo la kuihami na kuilinda nchi.
Ali Akbar Velayati, ameyasema hayo leo mbele ya waandishi wa habari na kusisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiombi ruhusa kwa yeyote kwa ajili ya kujilinda na kujihami; na mpango wa ulinzi wa Iran hauna uhusiano wowote na Marekani.
Dakta Velayati amebainisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitotetereshwa na mashinikizo ya kipropaganda; na kwa kuzingatia malengo iliyojiwekea, wakati wowote ule itakapoona inafaa itafanya majaribio mengine ya makombora.
Velayati ambaye pia ni Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wa Masuala ya Kimataifa amesema rais mpya wa Marekani anataka kuzusha hitilafu na kuwagawa walimwengu kimatapo na akasisitiza kwa kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonyesha kuwa haiwezi kuwekwa kando ya ulingo wa kimataifa kwa propaganda chafu na mashinkizo ya kipropaganda na kisaikolojia, bali itaendelea kuwepo kila siku na kwa nguvu zaidi katika ulingo huo.
Mafanikio yaliyopatikana katika mfumo wa makombora wa Iran yamewakasirisha maadui wa Jamhuri ya Kiislamu na hasa Marekani. Hii ni pamoja na kwamba viongozi wa Iran wamekuwa wakisisitiza kila mara kuwa uwezo wa makombora wa taifa hili unazingatia misingi maalumu ya kulinzi iliyoainishwa.../