Hoteli ya Abbasi Isfahan Iran, maridadi zaidi Mashariki ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i25902-hoteli_ya_abbasi_isfahan_iran_maridadi_zaidi_mashariki_ya_kati
Hoteli ya Abbasi mjini Isfahan nchini Iran imetangazwa kuwa, hoteli maridadi zaidi Mashariki ya Kati.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 03, 2017 23:52 UTC
  • Hoteli ya Abbasi Isfahan Iran, maridadi zaidi Mashariki ya Kati

Hoteli ya Abbasi mjini Isfahan nchini Iran imetangazwa kuwa, hoteli maridadi zaidi Mashariki ya Kati.

Katika taarifa kuhusiana na vivutio vya kitalii na hoteli katika eneo la Mashariki ya Kati au Asia Magharibi, Televisheni ya CNN  imesema Hoteli ya Abbasi katika mji wa kale wa Isfahan kati mwa Iran ni hoteli ya  aina yake.

Ripoti hiyo imesisitiza kuwa mji wa kale wa Isfahan una maajabu kadhaa ya kihistoria ambayo baadhi yamesajiliwa katika Orodha ya Turathi za Dunia ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO.

Mandhari za kuvutia za Hotel ya Abbasi

CNN imesema Hoteli ya Abbasi yenyewe sasa imekuwa kivutio cha kitalii kutokana na umaridadi wake wa kipekee.

Hoteli hiyo ilijengwa  miaka 300 iliyopita kwa muundo wa caravansary yaani sehemu ya wasafiri wa jangwani kupumzikia wakiwa katika safari zao za masafa marefu. Iliharibiwa katika vita mjini Isfahan lakini ikaendelea kuwepo na kubadilishwa kuwa kituo cha kijeshi wakati wa utawala wa silsila ya wafalme wa Qajari nchini Iran. Ikilarabatiwa muongo wa 1950 na kubadilishwa kuwa moja ya hoteli maridadi zaidi duniani. Hoteli hiyo yenye vyumba 250 imejengwa kwa usanifu majengo wa zama za Safavi na Qajari na ina kumbi 11.

Sekta ya utalii imekuwa ikiimarika nchini Iran katika miaka ya hivi karibuni baada ya kuondolewa vikwazo.