Rais Rouhani: Chaguzi nchini Iran hufanyika kwa uhuru, salama, ushindani na demokrasia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i26068-rais_rouhani_chaguzi_nchini_iran_hufanyika_kwa_uhuru_salama_ushindani_na_demokrasia
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, chaguzi nchini Iran hufanyika katika mazingira huru, salama, ya ushindani na kidemokrasia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 07, 2017 12:10 UTC
  • Rais Rouhani: Chaguzi nchini Iran hufanyika kwa uhuru, salama, ushindani na demokrasia

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, chaguzi nchini Iran hufanyika katika mazingira huru, salama, ya ushindani na kidemokrasia.

Rais Hassan Rouhani amesema hayo akijibu madai ya Marekani dhidi ya taifa hili na kusema kuwa, wale wanaokosoa chaguzi zinazofanyika hapa nchini wanapaswa kuangalia chaguzi zao pamoja na mambo yanayowahusu.

Rais Rouhani amesema kuwa, uchaguzi wa mwaka jana wa Marekani ulilalamikiwa na pande mbili na kabla ya uchaguzi huo Donald Trump Rais wa sasa wa nchi hiyo alikuwa na mashaka makubwa juu ya jinsi uchaguzi huo utakavyofanyika, hivyo basi Wamarekani wanapaswa kuziangalia chaguzi zao na kuangalia namna ya kufanya marekebisho kuhusu namna uchaguzi huo unavyofanyika.

Wananchi wa Iran wakishiriki katika moja ya chaguzi

Rais Hassan Rouhani ameongeza kuwa, wakati asilimia 70 mpaka 73 ya wananchi inapojitokeza na kushiriki katika uchaguzi, bila shaka inafahamika wazi kwamba, wananchi wana imani na uchaguzi.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani hivi karibuni ilitoa ripoti yake ya kila mwaka ya haki za binadamu ambapo kama kawaida ilitoa madai yasiyo na msingi wowote dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Jana Ayatullah Sadiq Amoli Larijani, Mkuu wa Idara ya Vyombo vya Mahakama nchini Iran akijibu ripoti hiyo ya Marekani alisema kuwa, Wamarekani ambao mikono yao imetapakaa damu kutokana na kutenda jinai dhidi ya haki za binadamu duniani kwa njia ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja hawana haki ya kutoa madai ya haki za binadamu dhidi ya Iran.