Iran iko tayari kwa ajili ya uchaguzi wa 19 Mei
Makamu wa Kwanza Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema serikali imejitayarisha kikamilifu kwa ajili ya kuandaa uchaguzii wa rais na uchaguzi mdogo wa bunge tarehe 19 Mei.
Akizungumza Jumatano alipotembelea makao makuu ya Idara ya Uchaguzi mkoani Kerman kusini mashariki mwa Iran, Is'haq Jahangiri amesisitiza kuwa, uchaguzi nchini Iran unazingatiwa kieneo na kimataifa.
Huku akiashiria hali nyeti katika eneo la Asia Magharibi na nara tata zinazotolewa na baadhi ya watawala wa Ulaya na Marekani amesema, kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi huu ni jambo litakaloonyesha nguvu na uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amesema kuna ushirikiano mzuri baina ya idara ya uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi.
Uchaguzi wa rais wa awamu ya 12 na uchaguzi wa duru ya tano ya mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji na pia uchaguzi mdogo wa 10 wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, utafanyika kwa pamoja Ijumaa tarehe 19 Mei mwaka huu.