Dahqan: Askari wa Marekani katika Ghuba ya Uajemi ni maharamia wajinga
Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu madai ya uongo yaliyotolewa na jeshi la Marekani akisema kuwa askari wa nchi hiyo walioko katika eneo la Ghuba ya Uajemi ni maharamia wajinga na majahili.
Brigedia Jenerali Hussein Dahqan amehoji kwamba, inawezekana vipi mwizi mwenye silaha aingie nyumbani kwako na atarajie kwamba utamtandikia zulia jekundu? Amesisitiza kuwa: Huu ni ujinga na ujahilia mamboleo wa karne ya 21.
Waziri wa Ulinzi wa Iran ameyasema hayo baada ya Kamanda wa majeshi ya Marekani, Joseph Votel kudai katika Kamati ya Jeshi ya Kongresi ya nchi hiyo kwamba meli za kivita za Iran zimekuwa zikitatiza na kulisumbua jeshi la majini la Marekani katika maji ya kimataifa.
Brigedia Jenerali Hahqan amohoji kwamba, Wamarekani wanafanya nini katika Ghuba ya Uajemi? Wanapaswa kuondoka katika eneo hili na kuacha kusababisha usumbufu na zahma kwa nchi za eneo hili.
Madai ya kamanda wa majeshi ya Marekani yametolewa baada ya manowari ya kubeba ndege za kivita ya Marekani kuingia katika maji ya Ghuba ya Uajemi na lango la Hormoz tarehe 23 mwezi huu wa Machi.