Iran haina wasi wasi kuhusu ibada ya Hija mwaka huu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i27618-iran_haina_wasi_wasi_kuhusu_ibada_ya_hija_mwaka_huu
Mwakilishi wa Faqihi Mtawala katika masuala ya Hija amesema, kufuatia mapatano yaliyotiwa saini baina ya Iran na Saudi Arabia, hakuna wasi wasi katika utekelezwaji ibada ya Hija mwaka huu kwa mahujaji wa Iran.
(last modified 2026-09-18T11:23:09+00:00 )
Apr 11, 2017 03:13 UTC
  • Iran haina wasi wasi kuhusu ibada ya Hija mwaka huu

Mwakilishi wa Faqihi Mtawala katika masuala ya Hija amesema, kufuatia mapatano yaliyotiwa saini baina ya Iran na Saudi Arabia, hakuna wasi wasi katika utekelezwaji ibada ya Hija mwaka huu kwa mahujaji wa Iran.

Hujjatul Islam wal Muslimin Qadhi Asghar, alisema hayo jana Jumatatu hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, ujumbe wa wataalamu kutoka Iran unaelekea Saudi Arabia kufuatilia utekelezwaji wa mapatano ya Tehran na Riyadh kuhusu Hija.

Mwaka jana Saudi Arabia kwa kutegemea madai ya uongo, iliwazuia mahujaji wa nchi kadhaa za Kiislamu zikiwemo Iran na Syria kutekeleza ibada ya Hija iliyofaradhishwa katika Uislamu.

Hatua hiyo ilifuatia baada ya Saudi Arabia kukosolewa vikali kutokana na msongamano mkubwa wakati wa ibada ya Hija ya mwezi Septemba 2015 katika eneo la Mina karibu na Makka ambapo duru zisizo rasmi zinasema Mahujaji 7,000 walipoteza maisha huku Saudia ikisisitiza ni watu 770 waliouawa katika msongamano huo. Iran ilitangaza kuwa mahujaji wake wapatao 465 walipoteza maisha katika maafa hayo ya Mina. Siku kadhaa kabla ya tukio hilo, Mahujaji 100 walipoteza maisha ndani ya Msikiti Mtakatifu wa Makka, wakiwemo Wairani 11 baada ya winchi kuwaangukia wakati wanatufu.

Hujjatul Islam wal Muslimin Qadhi Asghar, Mwakilishi wa Faqihi Mtawala katika masuala ya Hija

Wairani zaidi ya 85,000 wanatazamiwa kushiriki katika ibada ya Hija mwaka kulingana na mapatano yaliyofikiwa na Saudia mwaka huu.

Iran imeafiki wananchi wake waende kuhiji baada ya utawala wa Saudi Arabia kuahidi kutekeleza matakwa ya Iran ya kuandaa ibada ya Hija yenye hadhi na kwa kuzingatiwa misingi ya amani, izza na utukufu wa mahujaji.