Majina ya wagombea urais Iran yatajwa, kampeni za uchaguzi zaanza
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i28052-majina_ya_wagombea_urais_iran_yatajwa_kampeni_za_uchaguzi_zaanza
Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ya Iran, jana usiku alitangaza majina ya wagombea sita wa uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mara baada ya kutangaza majina hayo alisema kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 66 cha sheria ya uchaguzi ya Iran, kampeni za uchaguzi wa 12 wa Rais zimeruhusiwa kuanza.
(last modified 2025-12-01T10:34:25+00:00 )
Apr 21, 2017 04:15 UTC
  • Wagombea katika uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
    Wagombea katika uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ya Iran, jana usiku alitangaza majina ya wagombea sita wa uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mara baada ya kutangaza majina hayo alisema kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 66 cha sheria ya uchaguzi ya Iran, kampeni za uchaguzi wa 12 wa Rais zimeruhusiwa kuanza.

Mwandishi wa shirika la habari la IRIB amemnukuu Ali Asghar Ahmadi akisema hayo na kuongeza kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 66 cha sheria ya uchaguzi ya Iran, kampeni za uchaguzi huanza siku wanapotajwa wagombea waliotimiza masharti ya kugombea urais humu nchini.

Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, jana usiku liliwasilisha kwa Wizara ya Mambo ya Ndani majina ya wagombea sita waliotimiza masharti ya kugombea urais.

Majina ya wagombea hao ni kama ifuatavyo: Sayyid Mostafa Aqa-Mirsalim, Sayyid Mostafa Hashemi-Taba, Es'haq Jahangiri, Mohammad-Baqer Qalibaf, Seyyed Ebrahim Raeisi na Hassan Rouhani.

Ali Asghar Ahmadi, Mkuu wa Tume ya Uchaguzi Iran

 

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya Iran, kampeni za wagombea urais zinaanza tangu siku walipotangazwa rasmi wagombea hadi masaa 24 kabla ya kuanza zoezi la upigaji kura. Uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya tarehe 19 mwezi ujao wa Mei sambamba na uchaguzi wa tano wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji kote nchini Iran.

Ikumbukwe kuwa, kwa mujibu wa sheria za uchaguzi za Iran, vyombo vya dola ni marufuku kujiingiza kwenye masuala ya uchaguzi, kama ambavyo wagombea wote wanapewa haki sawa za kunadi sera zao. Vyombo vya habari vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama vile redio na televisheni vinatoa haki sawa kwa wagombea wote kwa kuhesabu hadi sekunde za kampeni za kila mgombea. Moja ya vigezo bora vya wagombea nchini Iran ni kutumia fedha chache zaidi katika kampeni zao za uchaguzi.