Iran: Katika matukio ya sasa Marekani iko katika nafasi dhaifu
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Ali Shamkhani amesema kuwa matukio ya sasa yameifanya Marekani kuwa katika nafasi dhaifu kwa kuwa hii leo nchi za Ulaya hazina tena mapenzi ya kushirikiana na Washington.
Shamkhani ameyasema hayo katika mahojiano na gazeti la Le Monde la Ufaransa wakati akibainisha siasa za Iran katika eneo la Mshariki ya Kati na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono uwekezaji wa mashirika ya Ulaya nchini hapa na kwamba vyanzo vya maliasili na gesi vya Iran ni fursa kwa ajili ya mashirikiano baina ya Iran na nchi hizo.
Akizungumzia hatua ya hivi karibuni ya Marekani likiwemo shambulizi lake la tarehe saba ya mwezi huu huko nchini Syria Shamkhani amesema kuwa, waungaji mkono wa Marekani katika eneo wanaizamisha nchi hiyo katika kinamasi cha migogoro; na Washington ingali inakariri makosa yake ya zamani. Amefafanua kuwa sambamba na Iran kulaani vikali shambulizi hilo la Marekani nchini Syria lililotekelezwa kwa kisingizio cha utumiwaji wa silaha za kemikali katika kijiji cha Khan Shaykhun, kusini mwa mkoa wa Idlib, Tehran inaamini kuwa, utumiwaji wa silaha hizo haukufanywa na serikali ya Damascus ambayo mwaka 2013 na kupitia mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Silaha za Kemikali ilizikabidhi silaha hizo kwa umoja wa Mataifa. Katika shambulizi la silaha za kemikali lenye kutia shaka hapo tarehe nne mwezi huu, kusini mwa mkoa wa Idlib, Syria zaidi ya watu 100 waliuawa na wengine karibu 400 walijeruhiwa.
Akizungumzia uingiliaji wa Washington nchini Syria, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, amesema kuwa akthari ya raia wa taifa hilo la Kiarabu wanaitambua serikali ya Rais Bashar al-Assad kuwa halali na ya kisheria kama ambavyo pia wanaiunga mkono. Kadhalika Wasyria wanaamini kuwa, mustakbali wa taifa lao unatokana na wao wenyewe bila ya uingiliaji wa kigeni.
Hayo yanajiri katika hali ambayo hivi karibuni afisa wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) Robert David Steele, alifichukua kuwa, utawala wa Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel zilishirikiana na viongozi wa Marekani katika njama ya shambulio la silaha za kemikali dhidi ya eneo la Khan Sheikhoun nchini Syria.