Iran ina haki ya kujibu jinai ya magaidi walioua askari wa mpakani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i28396-iran_ina_haki_ya_kujibu_jinai_ya_magaidi_walioua_askari_wa_mpakani
Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Hussein Dehqan amesema Jamhuri ya Kiislamu ina haki ya kutoa jibu kali kwa jinai ya magaidi ambao waliwaua askari wa kulinda mpaka katika eneo la kusini mashariki katika mpaka wa Iran na Pakistan.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Apr 29, 2017 03:08 UTC
  • Iran ina haki ya kujibu jinai ya magaidi walioua askari wa mpakani

Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Hussein Dehqan amesema Jamhuri ya Kiislamu ina haki ya kutoa jibu kali kwa jinai ya magaidi ambao waliwaua askari wa kulinda mpaka katika eneo la kusini mashariki katika mpaka wa Iran na Pakistan.

Akizungumza Ijumaa Dehqan ameongeza kuwa, Iran pia inaitaka Pakistan ichukue hatua za haraka za kuwakamata na kuwaadhibu magaidi hao. Aidha amesema Iran itafuatilia  kesi hiyo kupitia serikali ya Pakistan.

Kwa upande wake Mkuu wa Polisi ya Iran Brigedia Jenerali Hussein Ashtari amesema hujuma za magaidi nchini hazitapita bila jibu. Amesema maadui wa taifa la Iran wanapaswa kufahamu kuwa ukatili na ugaidi wao hautapita bila jibu.

Mazishi ya mmoja wa maafisa wa polisi aliyeuawa Jumatano katika mpaka wa Iran na Pakistan

Tayari Rais Hassan Rouhani wa Iran ameshamuandikia barua Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif akitaka waliotekeleza jinai hiyo wafikishwe kizimbani.

Itakumbukwa kuwa Jumatano usiku magaidi walihujumu nukta ya sufuri katika mpaka wa Iran na Pakistan na kuwaua shahidi maafisa wa polisi waliokuwa wakilinda doria katika eneo hilo mkoani Sistan Baluchistan. Kijikundi cha kitakfiri kijulikanacho kama 'Jaysh al Dhulm' kimetangaza kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi.