Abdolreza Rahmani Fazli: Pakistan imeahidi kudumisha usalama katika mipaka yake na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i28730-abdolreza_rahmani_fazli_pakistan_imeahidi_kudumisha_usalama_katika_mipaka_yake_na_iran
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Pakistan imeahidi kudumisha amani na usalama katika mipaka yake na Iran kwa shabaha ya kuzuia harakati za makundi ya kigaidi katika maeneo hayo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 06, 2017 09:02 UTC
  • Abdolreza Rahmani Fazli: Pakistan imeahidi kudumisha usalama katika mipaka yake na Iran

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Pakistan imeahidi kudumisha amani na usalama katika mipaka yake na Iran kwa shabaha ya kuzuia harakati za makundi ya kigaidi katika maeneo hayo.

Abdolreza Rahmani Fazli amesema hayo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari hapa mjini Tehran  ambapo ameashiria safari ya hivi karibuni ya Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Pakistan na kubainisha kuwa, viongozi wa Islamabad wameahidi kuchukua hatua madhubuhuti kuimarisha zaidi usalama katika mipaka yake na Iran ili kuzuia upenyaji wa makundi ya kigaidi yanayotokea nchini humo na kuja kufanya mashambulia ndani ya ardhi ya Iran.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  amesema pia kuwa, viongozi wa Pakistan wameahidi  kusaka na kuwatia mbaroni wanachama wa kundi la kigaidi lililotekeleza shambulio hivi karibuni katika mpaka wa Iran na kupelekea walinzi kadhaa wa mpaka kuuawa shahidi.

Eneo la mpakani katika ya Iran na Pakistan

Ikumbukwe kuwa, katika shambulio la magaidi la Aprili 26 ya mwezi uliopita katika mji wa Mirjaveh jirani na Pakistan walinzi 9 wa mpakani wa Iran waliuawa shahidi wakati walipokuwa katika doria yao ya kawaida. 

Kundi la Jeish al-Dhulm la Pakistan lilitangaza kuhusika na shambulio hilo. Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamekuwa wakiilalamikia mara kwa mara Pakistan kutokana na kutekelezwa mashambulio ya kigaidi dhidi ya ardhi ya Iran na makundi ya kigaidi yanayotokea upande wa Pakistan.