Iran kushiriki zaidi katika kuhuisha barabara ya hariri
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i29186-iran_kushiriki_zaidi_katika_kuhuisha_barabara_ya_hariri
Waziri wa Uchumi wa Iran Ali Tayyebnia amesema Iran itajihusisha zaidi katika kuhuisha Barabara ya Hariri.
(last modified 2026-09-17T07:35:18+00:00 )
May 16, 2017 23:18 UTC
  • Iran kushiriki zaidi katika kuhuisha barabara ya hariri

Waziri wa Uchumi wa Iran Ali Tayyebnia amesema Iran itajihusisha zaidi katika kuhuisha Barabara ya Hariri.

Tayyebnia aliyasema hayo Jumanne mjini Tehran baada ya kurejea kutoka China katika kikao kilichojadili uhuishwaji wa barabra ya kale ya hariri. Tayyebnia alisema kila mmoja anafahamu nafasi muhimu ya Iran katika kuhuisha barabara ya hariri.

Ameashiria kufanyika mkutano wa kimataifa huko Beijing China kujadili barabara ya hariri na kusema mkutano huo ulikuwa na umuhimu mkubwa . Mkutano wa "Ukanda Mmoja na Njia Moja"  ambao ni Ukanda wa Kiuchumi wa Njia ya Hariri ya Nchi Kavu na ya Baharini ulimalizika siku ya Jumatatu mjini Beijing kwa kuhudhuriwa na wajumbe 1,500 wakiwemo wageni 850 kutoka nchi 130.

Barabara ya Hariri ya nchi kavu na baharini

Mpango huo wa Ukanda Mmoja na Njia Moja ulizinduliwa na Rais Xi Jinping wa China mwaka 2013 kwa lengo la kuzinguanisha nchi za Asia, Afrika na Ulaya kwa kutumia njia ya kale ya barabara ya hariri ya karne za 16 na 18.

Jinping pia amesema, kiini cha pendekezo la "Ukanda Mmoja na Njia Moja" ni kuhimiza ujenzi wa miundombinu na maingiliano, kuunganisha sera na mikakati ya maendeleo ya nchi mbalimbali, kuimarisha ushirikiano wa kivitendo, na kuhimiza maendeleo ya pamoja, ili kutimiza ustawi wa pamoja.