Ashtari: Iran iko tayari kuzipatia uzoefu wa kipolisi nchi za Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i29584-ashtari_iran_iko_tayari_kuzipatia_uzoefu_wa_kipolisi_nchi_za_kiislamu
Mkuu wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kikosi cha polisi cha taifa hili kiko tayari kushirikiana na nchi zote katika nyuga zote husuasan katika suala la kupambana na uhalifu wa kimataifa.
(last modified 2025-10-31T09:05:42+00:00 )
May 25, 2017 13:57 UTC
  • Ashtari: Iran iko tayari kuzipatia uzoefu wa kipolisi nchi za Kiislamu

Mkuu wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kikosi cha polisi cha taifa hili kiko tayari kushirikiana na nchi zote katika nyuga zote husuasan katika suala la kupambana na uhalifu wa kimataifa.

Brigedia Jenerali Hossein Ashtari amesema hayo leo hapa mjini Tehran katika mazungumzo yake na Jenerali Tito Karnavian Mkuu wa Polisi ya Taifa ya Indonesia na kuongeza kuwa, inasikitisha kuona kwamba, nafasi mbaya na haribifu ya baadhi ya nchi  imepelekea kujitokeza makundi ya kigaidi likiwemo la Daesh ambayo yanachafua sura ya Uislamu.

Mkuu wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, madola ya kibeberu ulimwenguni daima yamekuwa yakifanya njama za kutia dosari sura safi ya Uislamu ambapo jeshi la polisi linapaswa kuwa na utendaji ambao utawakwamisha maadui katika kufikia njama zao.

Brigedia Jenerali Hossein Ashtari, Mkuu wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Hossein Ashtari amesema kuwa, Iran iko tayari kuzipatia uzoefu wake wa kipolisi nchi za Kiislamu ikiwemo Indonesia na kusisitiza kwamba, Iran inaweza kuipatia nchi rafiki na ya Kislamu ya Indonesia uzoefu wake katika kupambana na ugaidi, vita dhidi ya magendo ya madawa ya kulevya na uhalifu wa mtandaoni.

Kwa upande wake, Jenerali Tito Karnavian Mkuu wa Polisi ya Taifa ya Indonesia sambamba na kusifu nia njema ya polisi ya Iran ya kuongeza uhusiano na kutaka kuweko mabadilishano ya kitajiriba na kiuzoefu kati ya pande mbili amesema, Iran ikiwa nchi ya Kiislamu ina nafasi muhimu sana katika kuinua kiwango cha usalama wa Indonesia na kwamba hadi sasa haijasita hata kidogo kuisaidia nchi yake.