Putin akariri umuhimu wa Iran katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria
Kwa mara nyingine tena Rais Vladimir Putin wa Russia amesisitiza juu ya umuhimu na nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria.
Shirika la habari la Russia Today lenye makao yake mjini Moscow limemnukuu Putin akiyasema hayo katika mahojiano na gazeti la Le Figaro la nchini Ufaransa na kuongeza kuwa, Iran, Uturuki, Russia, serikali ya Syria pamoja na makundi ya kujitolea ya wananchi wa Syria yana umuhimu mkubwa katika kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu.
Kuhusu madai kuwa serikali ya Syria ilitumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake, Rais wa Russia amesema tuhuma hizo za nchi za Magharibi hazina ukweli wala msingi wowote na zimechochewa kisiasa.
Amesema madai hayo yalizushwa ili muungano wa kijeshi wa Marekani na waitifaki wake upate kizingizio cha kuhahalilisha uwepo wao wa kijeshi katika taifa hilo bila idhini wala baraka za serikali.
Rais Putin wa Russia amefafanua kuwa, Marekani ilifanya shambulizi dhidi ya Syria kwa madai hayo bandia, na kupuuza wito wa kuundwa kundi huru la uchunguzi lisilopendelea upande wowote kutoka taasisi ya kuzuia silaha za kemikali ili kubaini matukio ya eneo la Khan Shaykhun mkoani Idlib nchini Syria.