Kerry: Makubaliano ya JCPOA hayahitaji baraka za Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i30134-kerry_makubaliano_ya_jcpoa_hayahitaji_baraka_za_marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Marekani amesema makubaliano ya nyuklia ya Iran yanaweza kuendelea kusimama imara na kutekelezwa pasina na ushiriki wa Washington.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 06, 2017 23:18 UTC
  • Kerry: Makubaliano ya JCPOA hayahitaji baraka za Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Marekani amesema makubaliano ya nyuklia ya Iran yanaweza kuendelea kusimama imara na kutekelezwa pasina na ushiriki wa Washington.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, John Kerry amesema makubaliano hayo hayawezi kubatilika iwapo Rais Donald Trump wa Marekani atakata rufaa dhidi yake.

wakati huohuo Kerry ametahadharisha kuwa, kuiwekea Iran vikwazo vipya vya kiuchumi ni jambo la hatari. Amesema: "Hakuna insafu yoyote kuchukua hatua ambayo haitakuwa na manufaa na maslahi kwetu (Marekani). Kuiwekea Tehran vikwazo vipya kutawafanya wananchi wa taifa hilo wahisi kuwa makubaliano hayo ya mwaka 2015 hayana faida yoyote kwao."

Waziri huyo wa zamani wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amebainisha kuwa, kuwasukuma Wairani ukutani hakuna maslahi kwa Wamarekani na kwamba kitendo hicho huenda kikawa na taathira hasi kwa Marekani.

Rais Donald Trump wa Marekani

Hii ni katika hali ambayo, Rais Donald Trump amekuwa akipinga vikali makubaliano hayo yanayojulikana kama JCPOA yaliyofikiwa kati ya Iran na kundi la 5+1 mwaka 2015 na amekuwa akiyataja kama 'makubaliano mabaya zaidi duniani katika historia ya hivi karibuni.'

Kadhalika aliahidi kuyachana katika siku yake ya kwanza ya kuingia Ikulu ya White House, jambo ambalo mpaka sasa hajalifanya licha ya kupita zaidi ya siku 100 ofisini.