Brigedia Jenerali Jazayeri: Iran ina njia ya kuiadhibu Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i30652-brigedia_jenerali_jazayeri_iran_ina_njia_ya_kuiadhibu_marekani
Naibu Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran ina namna na njia ya kuiadhibu Washington baada ya Bunge la Seneti la Marekani kupasisha vikwazo vipya dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran IRGC kwa madai yasiyo na msingi ya ugaidi.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Jun 18, 2017 23:08 UTC
  • Brigedia Jenerali Jazayeri: Iran ina njia ya kuiadhibu Marekani

Naibu Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran ina namna na njia ya kuiadhibu Washington baada ya Bunge la Seneti la Marekani kupasisha vikwazo vipya dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran IRGC kwa madai yasiyo na msingi ya ugaidi.

Brigedia Jenerali Massoud Jazayeri ambaye pia ni Msemaji wa Majeshi ya Iran amesema uamuzi huo kwa mara nyingine tena umeudhihirishia ulimwengu kuwa, Marekani ni dola la kibeberu na la kiistikbari, na sifa hizo ndizo chimbuko la uhasama dhidi ya Iran.

Amesema: "Tangu miaka ya mwanzo ya Mapinduzi ya Kiislamu, taifa la Iran linafahamu vyema uhasama na uadui wa Marekani dhidi ya Mapinduzi, muundo na mashina yake yenye taathira kama vile Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran IRGC."

Alkhamisi iliyopita, Bunge la Seneti la Marekani lilipasisha vikwazo vipya dhidi ya Iran, hatua ambayo itapalelekea Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran IRGC kuwekewa vikwazo vya silaha.

Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran

Wakati huo huo, Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) itatoa jibu mwafaka kufuatia hatua hiyo ya kihasama ya Marekani.

Amesema kupasishwa vikwazo vipya dhidi ya Iran ni kitendo cha uhasama na kilicho kinyume cha sheria, sambamba na kuvunja moyo wa makubaliano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).