Jun 21, 2017 13:57 UTC
  • Spika Larijani: Kugawanywa Iraq ndilo takwa la utawala wa Kizayuni wa Israel

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza juu ya kudumishwa umoja wa Iraq na kubainisha kwamba, kugawanywa nchi hiyo ya Kiarabu ndilo takwa hasa la utawala wa Kizayuni wa Israel.

Dakta Ali Larijani amesema hayo leo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Haider Jawad Kadhim Al-Abadi Waziri Mkuu wa Iraq aliyeko hapa nchini kwa ziara rasmi. Larijani amesema kuwa, waungaji mkono wa magaidi wa Daesh wanatekeleza na kulinda maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unapanga njama za kuigawa Iraq ambayo ni nchi ya kidemokrasia na yenye taathira katika eneo la Mashariki ya Kati.

Amesema kuwa, maadui wanafanya njama za kuishughulisha Iraq na masuala ya ndani ili ighafilike na masuala ya nje ya mipaka yake.

Haider  Al-Abadi Waziri Mkuu wa Iraq

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza juu ya misimamo ya pamoja ya Tehran na Baghdad na kuongeza kuwa, kupambana na njama za kupigania kuigawa Iraq ni jambo muhimu sana na kwamba Jamhuri ya Kiislamu inalitambua suala hilo kuwa hatari kubwa.

Kwa upande wake Haider Jawad Kadhim Al-Abadi Waziri Mkuu wa Iraq amebainisha uhusiano imara wa Tehran na Baghdad na kubainisha kwamba, katu hautaingia dosari. Aidha amesema katika mazungumzo yake na Dakta Larijani kwamba, mshikamno baina ya mataifa mbalimbali kwa ajili ya kuliangamiza kundi la kigaidi la Daesh ni jambo la dharura mno.

Amesema, kuweko hitilafu miongoni mwa baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati kumekuwa kikwazo cha kutokomezwa kundi la kigaidi la Daesh.

 

 

Tags