UN yaipongeza Iran kwa kutoa huduma ziada kwa wakimbizi
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi UNHCR limeipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kutoa huduma ziada kwa wakimbizi.
Kwa mujibu wa mwakilishi wa UNHCR nchini Iran Sivanka Dana Pala, Iran ni nchi ya nne duniani yenye idadi kubwa zaidi ya wakimbizi na kuongeza kuwa, ukarimu wa Iran kwa wakimbizi ni mfano wa kuigwa na mataifa mengine. Akizungumza Jumatano kwa munasaba wa Siku ya Wakimbizi Duniani katika hafla iliyofanyika katika kambi moja ya wakimbizi mjini Mashhad kaskazini mashariki mwa Iran amesema kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi inayopenda amani na ubinadamu na hayo yanatokana na mafundisho ya Uislamu" Amesema Iran imewakirimu wakimbizi zaidi ya majukumu yake ya kimataifa.
Mwakilishi wa UNCHR nchini Iran ameongeza kuwa, kuadhimishwa Siku ya Wakimbizi Duniani katika miji mingi ya Iran ni jambo linaloashiria namna wakimbizi wanavyozingatiwa nchini hapa. Sivanka Dana Pala amesema Iran imekuwa ikiwapa wakimbizi huduma maalumu za kiafya, kimaisha na kielimu. Afisa huyo wa UNHCR amesistiza kuwa, Iran imewafungulia wakimbizi mipaka yake na kuwaruhusu wasome katika shule na vyo vikuu nchini kiasi kwamba wakimbizi wanahisi kupata suhula sawa na wananchi wa Iran.