Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds yaanza kote Iran
Maandamano ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds yameanza leo kote nchini Iran kwa kaulimbiu ya "Siku ya Kimataifa ya Quds; Nembo ya Umoja na Jihadi ya Umma wa Kiislamu, Uungajimkono kwa Wananchi Madhlumu wa Palestina na Kuangamizwa Utawala wa Kizayuni".
Leo Ijumaa wananchi wa Iran ya Kiislamu wamekusanyika kwa wingi kwa hamasa kubwa katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kutangaza uungaji mkono wako kwa mapambano ya kukomboa Quds Tukufu huku wakipiga nara za "Mauti kwa Marekani" na "Mauti kwa Ubeberu wa Dunia na Uzayuni wa Kimataifa" ili kuwafikishia na kuwatangazia walimwengu hasira na kuchukizwa kwao na mauaji ya kigaidi, kukaliwa kwa mabavu na mauaji ya halaiki yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina.
Mwishoni mwa marasimu hayo ya Siku ya Kimataifa ya Quds, washiriki watatoa azimio wakilaani jinai za utawala wa Kizayuni, kundi la kigaidi la Daesh pamoja na waitifaki wao wanaoongozwa na Marekani na kutangaza uungaji mkono wao kwa muqawama wa wananchi waliodhulimiwa wa Palestina.
Waandamanaji katika maeneo mbalimbali ya Iran wanaadhimisha Siku hii ya Quds kwa kuelekea katika maeneo ya misikiti kunapofanyika Swala ya Ijumaa. Jumla ya waandishi habari elfu nne wa ndani ya Iran na nje ya nchi wanaakisi maadhimisho haya ya Siku ya Kimataifa ya Quds kote nchini Iran.
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds yanafanyika pia katika nchi nyingine dunia.
Habari zaidi kuhusu maadhimisho hayo katika maeneo mbalimbali yaa dunia zitakujieni katika matangazo yetu yajayo.