Iran: Makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hayatafanyiwa mabadiliko yoyote
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i31182-iran_makubaliano_ya_nyuklia_ya_jcpoa_hayatafanyiwa_mabadiliko_yoyote
Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Kigeni ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa jina maarufu la JCPOA hayatofanyiwa marekebisho yoyote yale.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 30, 2017 23:34 UTC
  • Iran: Makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hayatafanyiwa mabadiliko yoyote

Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Kigeni ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa jina maarufu la JCPOA hayatofanyiwa marekebisho yoyote yale.

Alaeddin Boroujerdi alisema hayo jana kujibu matamshi ya mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa aliyedai kuwa nchi yake iko katika mchakato wa kuyaangalia upya makubaliano hayo. Boroujerdi amesema: JCPOA ni makubaliano ya kimataifa na kwamba suala la kuangaliwa upya makubaliano hayo si la nchi moja kama ambavyo pia hakuna mabadiliko yoyote yatakayofanyiwa makubaliano hayo.

Pande zilizotia saini makukbaliano ya JCPOA

 

Amesema, serikali ya rais wa Marekani Donald Trump ni ya wanagenzi kiasi kwamba inashindwa hata kujua kuwa JCPOA ni makubaliano ya kimataifa ya nchi kadhaa yaani upande mmoja ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na upande wa pili wa makubaliano hayo ni nchi sita pamoja na Umoja wa Ulaya.

Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Kigeni ya Majlisi ya ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ameongeza kuwa, inachopaswa kufanya Marekani ni kutekeleza majukumu yake kuhusiana na makubaliano ya JCPOA na iache siasa zake za kujikumbizia kila kitu upande wake na kujaribu kuvuruga makubaliano hayo muhimu kupitia kuweka vikwazo vipya. 

Amesema jambo moja liko wazi nalo ni kwamba hatua yoyote itakayochukuliwa na Marekani haiwezi kuachwa vivi hivi bila ya kupata majibu mfano wake kutoka kwa Iran.