Iran kushirikiana zaidi na Polisi ya Kimataifa, Interpol
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i31608-iran_kushirikiana_zaidi_na_polisi_ya_kimataifa_interpol
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Iran amesema nchi za Ulaya na Marekani zinadai kupambana na ugaidi lakini hazichukui hatua za kutosha katika kukabiliana na makundi ya kigaidi.
(last modified 2026-09-03T12:21:49+00:00 )
Jul 10, 2017 22:39 UTC
  • Iran kushirikiana zaidi na Polisi ya Kimataifa, Interpol

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Iran amesema nchi za Ulaya na Marekani zinadai kupambana na ugaidi lakini hazichukui hatua za kutosha katika kukabiliana na makundi ya kigaidi.

Mohammad Jaafar Muntadhari, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Iran ameyasema hayo leo mjini Tehran alipokutana na Jürgen Stock Katibu Mkuu wa Polisi ya Kimataifa, Interpol mjini Tehran na kuongeza kuwa: "Kijikundi cha kigaidi cha munafikin (MKO) ambacho shughuli zake zimeratibiwa kimehusika na hujuma za kigaidi ambazo zimepelekea idadi kubwa ya maafisa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuuawa shahidi lakini leo nchi za Magharibi na hasa Marekani zimeiondoa MKO katika orodha ya makundi ya kigaidi na hata kuipa nguvu".

Muntadhari amekosoa wanaodai kupambana na ugaidi  katika hali ambayo wanaunga mkono ugaidi na kusema: "Katika kipindi cha miaka 38, Iran imepata uzoefu wenye thamani katika vita dhidi ya ugaidi na kwamba iko tayari kuipa jamii ya kimataifa uzoefu huo."

Mkutano wa kimataifa wa Polisi ya Iran na Polisi ya Kimataifa, Interpo, Tehran 2017,10,07

Amesema Interpol ni daraja katika vita dhidi ya ugaidi katika uga wa kimataifa na kuongeza kuwa Polisi ya Iran iko tayari kushirikiana na Interpol. Amesema mwaka jana Iran ilifuatilia faili 16,665 za Interpol na kuwakabidhi raia 30 wa kigeni kwa polisi hiyo ya kimataifa. Aidha Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Iran ameitaka Interpol kufuatilia wahalifu ambao Iran imetaka wakamatwe kimataifa na kuwakabidhi kwa vyombo vya mahakama vya Iran.

Kwa upande wake Jürgen Stock Katibu MKuu wa Interpo amesema Iran iko mstari wa mbele katika vita dhidi ya ugaidi. Amesema hatua ilizochukua Iran katika vita dhidi ya biashara ya mihadarati ni jambo ambalo limepelekea  Iran na nchi zingine kupata utulivu. Aidha ameashiria ushirikiano wa Iran na Interpol katika kukabiliana na uhalifu wa mitandano ya intaneti na kusema, Interpol inaunga mkono Iran katika uga huo.