Marekani yakiri Iran imeheshimu makubaliano ya nyuklia
Serikali ya Marekani imetangaza kuwa, Iran imeheshimu makubaliano ya nyuklia yaliyotiwa saini baina ya Tehran na kundi la 5+1 maarufu kwa jina la makubaliano ya JCPOA.
Mtandao wa Intaneti wa redio ya NPR ya nchini Marekani umeandika kuwa, Rex Tillerson, waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, jana Jumatatu alisisitiza kuwa, Iran imehehimu makubaliano ya nyuklia na inatekeleza vipengee vya Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja kwa kifupi JCPOA.
Hata hivyo redio ya NPR imewanukuu viongozi wa White House wakidai kuwa, Iran ni tishio kubwa la manufaa ya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.
Serikali ya Marekani ina jukumu la kuwasilisha ripoti kwa Baraza la Congress, kuhusiana na kuheshimu Iran makubaliano hayo ya nyuklia kila baada ya siku 90.
Licha ya serikali ya Donald Trump kupinga makubaliano hayo, lakini hii ni mara ya pili inalazimika kukiri kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeheshimu ahadi zake katika Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA).
Ben Rhodes, mshauri wa rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama amesema kuwa, serikali ya Trump haiwezi kukwepa uhakika kwamba Iran inaheshimu makubaliano hayo ya nyuklia, kwani Tehran inahakikisha haitoi mwanya wowote wa kulaumiwa kuhusu utekelezaji wa JCPOA.
Marekani imeshadidisha siasa zake zilizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya kuingia madarakani Donald Trump, rais mwenye matatizo mengi wa nchi hiyo.
Makubaliano ya nyuklia yaliyopewa jina la Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA) yaliyofikiwa baina ya Iran na kundi la 5+1 linaoundwa na Russia, China, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Marekani pamoja na Umoja wa Ulaya, yalianza kutekelezwa mwezi Januari 2016, lakini mara zote Marekani imekuwa ikivunja waziwazi makubaliano hayo.