Boroujerdi: Marekani inapasa kuheshimu makubaliano ya kimataifa
Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kuwa Marekani inapasa kujifunza maadili ya kisiasa kuhusu makubaliano ya kimataifa na kuheshimu makubaliano hayo.
Allauddin Boroujerdi leo ameashiria vikwazo vipya vya Marekani na hatua za bunge la Iran katika uwanja huo na kuongeza kuwa Kamisheni ya Usalama wa Taifa ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran imeandaa mpango wake wa awali wa kukabiliana na vikwazo hivyo na kwamba mpango huo utafuata mkondo wa kisheria.
Boroujerdi ameongeza kuwa bunge la Iran tarehe 29 mwezi huu wa Julai litachunguza katika kikao chake cha dharura wiki ijayo mapendekezo yaliyotolewa na wabunge wa Iran ambayo lengo lake ni kutoa jibu la wazi na kali kwa Congresi ya Marekani.
Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliunga mkono makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa na kusisitiza kuwa kuingia madarakani serikali mpya huko Marekani hakupasi kutilia shaka na kukiuka vipengee vya makubaliano hayo baada ya kufanyika mazungumzo magumu ya miezi kadhaa yaliyozijumuisha nchi sita zilizosaini makubaliano hayo. Congresi ya Marekani juzi usiku iliidhinisha kwa kura 419 za ndio mpango wa kuiwekea Iran vikwazo vipya ikiwa ni katika kuendelea mwenendo wa chuki na kiuhasama wa Washington dhidi ya Tehran.