Iran yawatia mbaroni makumi ya magaidi wa Daesh/ISIS
Vyombo vya usalama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimewakamata wanachama 27 wenye mfungamano na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) waliokuwa wanapanga njama ya kutekeleza mashambulizi ya kigaidi nchini.
Wizara ya Intelijensia ya Iran imesema magaidi hao walikuwa wanajiandaa kufanya hujuma za kigaidi katika mikoa ya nchi na miji ya kidini hapa Iran kuelekea sherehe za kuapishwa Rais Hassan Rouhani Jumamosi iliyopita.
Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa, magaidi 10 miongoni mwao walikamatwa ndani ya ardhi ya Iran na wengine 17 walitiwa nguvuni nje ya nchi pamoja na silaha za kijeshi na mada za miripuko walizotaka kuziingiza nchini.
Taarifa hiyo imetolewa siku moja baada ya Brigedia Jenerali Mohammad Pakpour, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC kusema kuwa wamefanikiwa kusambatarisha mtandao wa kigaidi uliokuwa na nia ya kuvuruga usalama wa taifa katika mpaka wa kaskazini magharibi mwa nchi.

Ikumbukwe kuwa, kufuatia jinai ya kigaidi iliyofanywa tarehe 7 ya mwezi wa Juni mwaka huu hapa mjini Tehran na kusababisha kuuawa shahidi kimadhulumu watu 18 na kujeruhiwa wengine 52, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC lilitangaza kuwa halitoruhusu kumwagwa damu takasifu pasina kutoa jibu kwa umwagaji damu huo.
Katika mashambulio ya makombora ya jeshi hilo dhidi ya maeneo ya magaidi wa Daesh katika eneo la Deir Ezzor nchini Syria, zaidi ya wanachama 170 wa kundi hilo la kitakfiri waliangamizwa.