Huenda uchumi wa Afrika ukaporomoka kutokana na vita dhidi ya Iran
Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, pamoja na Umoja wa Afrika na Benki ya Maendeleo ya Afrika, yametoa ripoti mpya ikionya kuwa uchumi wa mataifa ya bara hili unaweza kukumbwa na kuporomoka ikiwa mapigano yanayoendelea katika ukanda wa Asia Magharibi yataendelea bila suluhu ya haraka.
Kwa mujibu wa taarifa ya Reuters , taasisi hizo zimesema kuwa kuendelea kwa vita kutasababisha ucheleweshaji wa muda mrefu na vurugu katika biashara, usambazaji wa nishati na pembejeo za kilimo—athari ambazo zitaenea kote barani Afrika.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa endapo mgogoro huo katika Asia Magharibi utaendelea kwa zaidi ya miezi sita, uchumi wa Afrika unaweza kupoteza hadi asilimia 0.2 ya ukuaji wa pato la taifa (GDP) kufikia mwaka 2026.
Rripoti hiyo iliyowasilishwa katika kikao cha Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa ambacho kimefanyika nchini Morocco, inaonya kuwa kadiri mgogoro unavyoendelea na kadiri usumbufu katika njia za usafirishaji, upatikanaji wa nishati na mbolea unavyoongezeka, ndivyo hatari ya kupungua kwa kasi kubwa ya uchumi barani Afrika inavyoongezeka.
Ingawa ripoti haikutoa takwimu mahsusi kuhusu athari za uwezekano wa kuongezeka kwa mfumuko wa bei, imeonya kuwa mgogoro huo unaweza haraka sana kugeuka kuwa janga la gharama za maisha kutokana na kupanda kwa bei za mafuta na chakula.
Hayo yanatajwa katika muktadha ambao Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) inashika asilimia 15.8 ya uagizaji wa bidhaa wa Afrika na asilimia 10.9 ya mauzo ya nje ya bara hili.
Wakati huohuo, nchi chache kama Nigeria, ambayo hivi karibuni imefunguwa kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta, na Msumbiji, muuzaji mkubwa gesi ya LNG, inaweza kunufaika na ongezeko la bei katika masoko ya kimataifa.
Mashambulizi ya kijeshi ya pamoja ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yalianza tarehe 28 Februari sawa na tarehe 10 ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na hadi sasa bado yanaendelea.
Kwa mujibu wa haki ya kimsingi ya kujilinda, iliyobainishwa katika Kifungu cha 51 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikijibu mashambulizi hayo ndani ya mfumo wa kuzuia uendelezaji wa uvamizi na kuongeza gharama kwa wavamizi, kwa kulenga kwa umakini ngome za kijeshi na kiusalama za utawala wa Kizayuni wa Israel katika maeneo mbalimbali ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, pamoja na kambi na vituo vya majeshi ya Marekani katika nchi za eneo.
Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia wametahadharisha kuwa kuendelea au kupanuka kwa uvamizi huo kutakabiliwa na majibu makali zaidi, madhubuti na ya upana mkubwa.