Iran: US ijiandae kwa matokeo mabaya ikikiuka JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i32906-iran_us_ijiandae_kwa_matokeo_mabaya_ikikiuka_jcpoa
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitahadharisha Marekani na matokeo mabaya itakayoyapata iwapo itaamua kukiuka makubaliano ya nyuklia ya Vienna.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 09, 2017 03:08 UTC
  • Iran: US ijiandae kwa matokeo mabaya ikikiuka JCPOA

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitahadharisha Marekani na matokeo mabaya itakayoyapata iwapo itaamua kukiuka makubaliano ya nyuklia ya Vienna.

Mohammad Javad Zarif alikiambia kikao cha Kamati ya Bunge ya Masuala ya Usalama wa Taifa na Sera za Nje jana Jumanne kuwa, kamwe Iran haitoruhusu Marekani ikwepe kutekeleza makubaliano hayo yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) kwa gharama na madhara ya taifa hili.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema lengo la Rais Donald Trump wa Marekani kusaini sheria ya vikwazo vipya dhidi ya Tehran ni kutaka kusambaratisha makubaliano hayo kwa kuisukuma Iran ukutani.

Baadhi ya viongozi walioshiriki kusainiwa JCPOA huko Vienna, Julai 2015

Dakta Zarif ameionya Marekani na kuitaka ijiandae kwa taathira hasi za kukiuka makubaliano hayo yaliyofikiwa Julai mwaka 2015 kati ya Iran na nchi wanachama wa kundi la 5+1 huko Vienna, Austria.

Iran imekuwa ikilalamikia mwenendo na misimamo ya Marekani katika suala la utekelezaji wa JCPOA, tangu makubaliano hayo yaanze kutekelezwa Januari mwaka jana 2016.