Zarif: Iran inakaribisha kubadilika sera za kieneo za Saudi Arabia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Ikiwa Saudi Arabia itaangalia upya siasa na sera zake za eneo la Mashariki ya Kati itapata jibu na radiamali chanya ya Jamhuri ya Kiislamu.
Mohammad Javad Zarif ameashiria kuwa Iran imekuwa daima ikitaka iwe na uhusiano mzuri na majirani zake na kubainisha kuwa sera za Iran katika kuamiliana na nchi za eneo ikiwa na pamoja na Saudia zimekuwa zikifuata muelekeo huo na wala hazijabadilka.
Zarif ameweka bayana kwamba kwa mtazamo wa Iran siasa na sera za Saudi Arabia katika eneo zimekuwa haribifu na za ubomoaji na hata matokeo yake yamekuwa ni kwa madhara ya nchi hiyo.
Kuhusu ombi lililotolewa na Saudia kwa Iraq kutaka iwe mpatanishi baina ya Iran na Saudia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Saudia inapaswa ibadilishe na kuangalia upya baadhi ya sera zake; na kufanya hivyo kutakuwa ni kwa maslahi ya taifa ya nchi hiyo.
Dakta Zarif ameashiria pia kwamba Iran imekuwa ikitangaza kila mara kuwa iko tayari kufanya na mazungumzo na Saudia na kueleza kuwa Jamhuri ya Kiislamu imekuwa kila mara ikitafuta utatuzi wa kisiasa wa migogoro ya eneo lakini ni jambo la kusikitisha kuwa Saudi Arabia haijafanya hivyo bali imekuwa ikifuatilia maslahi yake kwa njia za kuzusha mivutano katika eneo hili.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu inatilia mkazo kuwepo Mashariki ya Kati yenye amani, yenye nguvu na ya mataifa yenye muelekeo wa pamoja na inaitakidi kuwa kuthibiti kwa jambo hilo ni kwa maslahi yake ya taifa na eneo kwa ujumla.../