Aug 30, 2017 07:26 UTC
  • Rais Rouhani: Iran sio itakayoanza kukiuka makubaliano ya nyuklia

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran sio itakayoanza kukiuka makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa jina la Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA).

Rais Rouhani amesema hayo katika mahojiano mubashara alipokuwa akizungumza na taifa kwa njia ya Televisheni na kusema kuwa, ni jambo lilo mbali kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomikia IAEA kuathiriwa na mashinikizo ya Marekani na hivyo kukubali ombi la Washington la kutaka kukaguliwa vituo vya kijeshi vya Iran.

Sambamba na kuashiria kwamba, Wamarekani wenyewe hawawezi kumtathmini Rais Donald Trump wa nchi hiyo na kuongeza kuwa, Iran haitakuwa taifa la kwanza kukiuka makubaliano ya nyuklia.

Rais Hassan Rouhani katika mahojiano maalumu

Hata hivyo Rais wa Iran amesema bayana kwamba, kama taifa lolote litakiuka makubaliano hayo, basi Tehran itatoa jibu linalofaa kwa ukiukaji huo. Rais Rouhani amesisitiza kwamba, kwa sasa Iran ina mazingira bora kabisa na Marekani iko katika hali mbaya kabisa na kuongeza kwamba, wakati ambapo Marekani inaliwekea vikwazo taifa hili, benki za kigeni zimekuwa zikitia saini makubaliano ya ushirikiano na taifa hili.

Kuhusiana na mgogoro wa uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia, Rais Rouhani amesisitiza kwamba, tatizo kuu ni uingiliaji wa Saudi Arabia huko Yemen na hatua yake ya kuunga mkono operesheni za kigaidi.

Rais Rouhani amesema kinagaubaga kwamba, kama Saudia itaacha kuingilia masuala ya ndani ya Yemen na kuwaachia Wayemen mambo yao na wakati huo huo ikaacha kuwaunga mkono magaidi, yumkini katika mazingira kama haya tofauti zilizopo kati ya pande mbili zikapatiwa ufumbuzi.

 

 

Tags