Iran: Marekani inafuatilia maslahi yake tu katika Mashariki ya Kati
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema baadhi ya nchi za eneo na Marekani zinatumia baadhi ya misamiati kwa ajili ya kufanikisha malengo na maslahi yao.
Bahram Qassemi ameyasema hayo leo mbele ya waandishi wa habari wa ndani na nje ya nchi wakati akijibu suali la mwandishi wa habari wa kitengo cha matangazo ya ngámbo ya IRIB kuhusu madai hewa aliyotoa Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia dhidi ya Iran baada ya mazungumzo ya simu aliyofanya hivi karibuni Rais wa Marekani na viongozi wa Riyadh. Qassemi amesema: Ushawishi wa Iran katika eneo ni suala la kimaumbile na lililo wazi kabisa kwa sababu utamaduni na ustaarabu si vitu vinavyoishia kwenye mipaka ya kijiografia, hivyo yale yanayojiri kwenye eneo linaloizunguka Iran ni suala la athari za ustaarabu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa "kueneza hofu kuhusiana na Iran" ni silaha butu na iliyopitwa na wakati na kusisitiza kwamba kutumia misamiati ya kuonyesha kuwa na wasiwasi juu ya ushawishi wa Iran ni siasa ghalati zinazotumiwa na baadhi ya nchi ili kuitenga Iran na eneo la Mashariki ya Kati na kisha kuyapa fursa madola ajinabi kuja kupora na kusomba hazina za mataifa ya eneo hili.
Kuhusu madai ya gazeti la Daily Telegraph linalochapishwa London, Uingereza kwamba Iran imeisaidia Korea Kaskazini katika uundaji makombora, Dakta Qassemi amesema madai hayo hayana maana, ya kupuuzwa na kuyazungumzia pia ni kupoteza wakati.
Kuhusu suali kwamba inasemakana Marekani imejitoa kwenye mkataba wa nyuklia wa JCPOA na kwamba kama ni hivyo Iran inayaangaliaje makubaliano hayo bila ya kuwemo Marekani, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Endapo nchi itakwepa kwa sababu yoyote ile kutekeleza ahadi ilizotoa italazimika kulipa mzigo wa gharama za matokeo ya kuhalifu kwake kutekeleza ahadi hizo.../