Gholamali Khoshroo: Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vinakiuka makubaliano ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i34361-gholamali_khoshroo_vikwazo_vya_marekani_dhidi_ya_iran_vinakiuka_makubaliano_ya_jcpoa
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesaema kuwa, vikwazo vya aina yoyote vinakiuka msingi wa diplomasia na mazungumzo na haviwezi kusaidia chochote katika kupeleka mambo mbele.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 14, 2017 22:57 UTC
  • Gholamali Khoshroo: Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vinakiuka makubaliano ya JCPOA

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesaema kuwa, vikwazo vya aina yoyote vinakiuka msingi wa diplomasia na mazungumzo na haviwezi kusaidia chochote katika kupeleka mambo mbele.

Kwa msingi huo amebainisha kwamba, serikali ya Marekani inapaswa kuachana na hatua zake za kutumia vikwazo kama wenzo wake katika siasa zake za kigeni.

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amezungumzia vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran na kusema kuwa, kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) Marekani iliahidi kuyalinda makubaliano hayo na ikasimamisha vikwazo vyake vya huko nyuma dhidi ya taifa hili.

Wawakilishi katika mazungumzo ya nyuklia ya Iran na kundi la 5+1

Gholamali Khoshroo ameongeza kuwa, kila mara unapowadia wakati wa kuviongezea muda wa kuvisimamisha vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran, ili Wamarekani waionyeshe Kongresi na wananchi wa nchi hiyo kwamba wana misimamo mikali huongezea katika orodha ya vikwazo majina ya watu kadhaa kwa madai yasiyo na msingi na kudai kwamba, vikwazo hivi vipya si vya kinyuklia.

Ikumbukwe kuwa, jana serikali ya Marekani sambamba na kuiwekea vikwazo vipya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ilitangaza kurefusha muda wa kusimamisha vikwazo vya nyuklia dhidi ya Tehran kwa kipindi kipingine cha miezi minne. 

Kwa mujibu wa tangazo la Wizara ya Hazina ya Marekani, serikali ya Washington imewawekea vikwazo vya kiuchumi shakhsia 11 na mashirika ya Kiirani na yasiyo ya Kiirani kwa sababu ya kuliunga mkono Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na madai ya kushiriki katika hujuma dhidi ya mfumo wa mawasiliano ya kompyuta dhidi ya Benki za Marekani.