Iran iko tayari kukabiliana na chokochoko yoyote ya Marekani
Afisa wa ngazi za juu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonya kuwa, iwapo Markeani itakiuka mapatano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Uteekelzaji, JCPOA, Iran iko tayari kuanza upya shughuli zake zote za nyuklia.
Afisa huyo wa ngazi za juu ambaye hakutaka jina lake litajwe ametoa kauli hiyo baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kusema tayari ameshachukua maamuzi kuhusu mapatano ya nyuklia baina ya Iran na madola sita makubwa duniani maarufu kama JCPOA. Afisa huyo amesema Iran iko tayari kukabiliana na uamuzi wowote ule utakaochukuliwa na Marekani.
Itakumbukwa kuwa Iran na nchi za 5+1 ambazo ni Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Marekani pamoja na Ujerumani zilitiliana saini mapatano ya nyuklia Julai 14 mwaka 2015 na kuanza kuyatekeleza Januari 16 mwaka jana.
Hata hivyo utawala wa Trump umekiuka ahadi za Marekani katika mapatano hayo na mtawala huyo pia amesema nchi yake itajiondoa katika mkataba huo wa kimataifa. Hii ni katika hali ambayo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki umesisitiza mara kadhaa katika ripoti zake kuwa Iran imefungamana kikamilifu na ahadi zake katika mapatano hayo na hivyo hakuna haja ya kuyabatilisha.