Qassemi: Sura bora ya Iran imedhihirishwa katika Umoja wa Mataifa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i34837-qassemi_sura_bora_ya_iran_imedhihirishwa_katika_umoja_wa_mataifa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu huko New York na kushiriki kwake katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kumedhirisha sura bora kuhusu siasa za Iran katika eneo na ulimwenguni kwa ujumla.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 25, 2017 11:14 UTC
  • Qassemi: Sura bora ya Iran imedhihirishwa katika Umoja wa Mataifa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu huko New York na kushiriki kwake katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kumedhirisha sura bora kuhusu siasa za Iran katika eneo na ulimwenguni kwa ujumla.

Akijibu swali kutoka kwa mwandishi wa kitengo cha matangazo ya ng'ambo cha Sauti na Televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu udiplomasia hai wa Iran huko New York na jitihada za Marekani za kuzusha mkondo wa tuhuma na madai kwamba Iran ni tishio katika eneo hili, Bahram Qassemi amebainisha kuwa mashauriano ya kisiasa iliyofanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini New York yalikuwepo kwa kiasi kikubwa tangu mwanzo wa Baraza Kuu la UN na yangali yanaendelea. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameyasema hayo leo katika kikao na waandishi habari wa ndani na  nje hapa Tehran. 

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje katika mkutano na waandishi wa habari wa ndani na nje jijini Tehran 

Qassemi ameongeza kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anaendelea kufanya mashauriano huko New York na hadi kufikia jana alikuwa ameshafanya mazungumzo, vikao na mahojiano na vyombo vya habari zaidi ya 42 huko New York; na kwamba mchakato huo utaendelea pia  siku sijazo.

Kuhusu siasa na matamshi dhidi ya Iran yaliyotolewa na Rais wa Marekani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kuwa, sera za Marekani hazina jipya na kwamba matamshi hayo yanadhihirisha wazi sura halisi ya serikali iliyopo madarakani. Kuhusu siasa mpya za serikali ya Marekani za kuwazuia raia wa Iran kuingia Marekani, Qassemi ameongeza kuwa hatua hiyo inayofuatiliwa na Rais wa Marekani si ya kibinadamu wala kimantiki na inapasa kulaaniwa.  

Alipoulizwa swali kuhusu kikao cha kamisheni ya pamoja ya makubaliano ya JCPOA  kwamba je, Jamhuri ya Kiislamu imewasilisha malalamiko yake kuhusu mchakato wa utekelezaji wa makubabaliano hayo, Bahram Qassemi amejibu kuwa, vikao viwili katika ngazi ya wataalamu na Mawaziri wa Mambo ya Nje vimefanyika New York na kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezungumzia vizuizi, ahadi mbaya na matatizo yote yaliyosababishwa na Marekani baada ya kufikiwa makubaliano hayo na kuongeza kuwa masuala hayo yote yatashughulikiwa.