Dakta Zarif aionya Marekani kuhusu kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, endapo Marekani itajitoa katika makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), basi Tehran nayo ina machaguo mengine ambayo inaweza kuyatekeleza.
Dakta Muhammad Javad Zarif amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na Kanali ya Televisheni ya al-Jazeera ya Qatar na kueleza bayana kwamba, endapo Marekani itaheshimu na kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya JCPOA itakuwa katika nafasi nzuri.
Makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA kwa kifupi yalifikiwa kati ya Iran na kundi la 5+1 linalozijumuisha nchi za Uingereza, Marekani, Russia, China, Ufaransa pamoja na Ujerumani na yalianza kutekelezwa Januari mwaka jana.
Hata hivyo Marekani ambayo ni miongoni mwa nchi zilizotia saini makubaliano hayo ya kihistoria imekuwa ikikwepa kutelekeza ahadi zake kuhusiana na makubaliano hayo na hivi sasa ni mtuhumiwa mkuu wa ukwamishaji utekelezaji wa makubaliano hayo.
Aidha katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kubainisha kwamba, siasa za Saudia mkabala na Qatar sio chanya amesisitiza kuwa, utawala wa Riyadh unapaswa kusitisha usambazaji na uenezaji ugaidi na fikra za kuchupa mipaka.
Dakta Zairif amesisitiza pia kwamba, Iran inaendelea na juhudi zake za kuhakikisha amani na uthabiti vinapatikana katika Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa, hatua za viongozi wa Saudia na Imarati zimekuwa na taathira hasi kwa juhudi hizo za Iran.