Ayatullah Khatami: Viongozi wa eneo la Kurdistan wamefanya hiana kubwa
Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran, Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesema kuwa, kitendo cha viongozi wa eneo la Kurdistan ya Iraq kutosikiliza nasaha za serikali kuu ya Iraq na nchi za eneo na kisha kuitisha kura ya maoni ya kutaka kujitenga, ni hiana.
Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami ameyasema hayo katika hotuba ya swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo mjini Tehran ambapo sambamba na kubainisha kwamba, nchi zote za dunia haziitambui rasmi kura hiyo ya maoni ya kutaka kujitenga eneo hilo, amesema kuwa, ushirikiano wa Iran, Iraq na Uturuki ni njia athirifu kwa ajili ya kukabiliana kwa dhati na njama za kura hiyo ya maoni.
Aidha imamu wa muda wa swala ya Ijumaa mjini Tehran amelaani shambulizi la hivi karibuni la kigaidi na mauaji ya watu wasio na hatia huko mjini Las Vegas, Marekani na kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani mauaji yoyote yanayotokea duniani dhidi ya watu wasio na hatia, lakini pia inaamini kuwa, Marekani na Wamagharibi kwa ujumla ni lazima wahitimishe undumakuwili wao kuhusiana na mauaji ya watu wasio na hatia kote duniani ikiwemo Yemen. Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran ameashiria ukiukaji wa msingi wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA unaofanywa na Washington na kusisitiza kuwa, makubaliano hayo hayatajadiliwa tena kama ambavyo raia wa Iran na viongozi wa nchi hii hawana imani hata kidogo na Marekani.

Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami ameashiria kuanza kwa Wiki ya Jeshi la Polisi nchini Iran na kusema kuwa, jeshi la polisi ni msingi wa izza na heshima ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuwa daima limekuwa mstari wa mbele katika kudhamini usalama na kupambana na viashiria vya ukosefu wa usalama, madawa ya kulevya na magendo ya bidhaa.