Pezeshkian: Iran haijapokea ujumbe wowote kutoka Marekani
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu haijapokea ujumbe wowote kutoka Washington hadi sasa.
Akijibu swali kuhusu iwapo serikali mpya ya Marekani imeitumia ujumbe wowote Jamhuri ya Kiislamu, Pezeshkian amewaambia waandishi wa habari kwamba, "Hapana, hatujapokea ujumbe hadi sasa."
Hivi karibuni, katika mahojiano maalum na Sky News katika mji mkuu wa Iran, Tehran, Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araghchi alisema kuwa, ingawa yuko tayari kumsikiliza (Rais wa Marekani, Donald) Trump, itachukua mengi zaidi ya hapo kwa Iran kushawishika kuwa inapaswa kuanza mazungumzo na Marekani kuelekea makubaliano, kutokana na kile kilichotokea huko nyuma.
Amesema, "Hali ni tofauti na ngumu zaidi kuliko wakati uliopita. Mambo mengi yanapaswa kufanywa na upande wa pili ili kununua imani yetu. Hatujasikia chochote isipokuwa neno 'zuri', na hii haitoshi."

Makubaliano ya JCPOA yalitiwa saini mwaka 2015 kati ya Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani.
Trump katika muhula wake wa kwanza alijiondoa kinyume cha sheria katika makubaliano hayo mwaka 2018. Russia, Uingereza, Ujerumani, China, Marekani na Ufaransa zimekuwa katika mazungumzo na Iran tangu Aprili 2021 ili kurejesha makubaliano hayo, bila mafanikio.