Tanzania na Iran zakubaliana kuunda kamisheni ya pamoja ya kiuchumi
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimefikia makubaliano ya kuunda kamisheni ya pamoja ya kiuchumi.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika mazungumzo ya Dakta Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na mwenzake Augustine Mahiga Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mazungumzo ambayo yalifanyika leo hapa mjini Tehran.
Katika mazungumzo hayo, mawaziri hao wa mashauri ya kigeni wa Iran na Tanzania wametangaza kuwa, nchi zao zilitoa kipaumbele katika ushirikiano kwenye nyanja za kibenki, kibalozi, utalii, elimu, teknolojia, maji na nishati.
Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, sekta binafsi na ya serikali ziko tayari kustawisha ushirikiano na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha Dakta Zarif amesisitiza katika mazungumzo yake na balozi Mahiga kwamba, Jamhuri ya kiislamuu ya Iran ina azma thabiti ya kukuuza na kustawisha zaidi ushirikiano wake na nchi za Kiafrika ikiwemo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wake, Augustine Mahiga Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesifu nafasu muhimu ya Iran katika nyuga mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, kielimu na kiutamaduni na akatoa wito wa kuimarishwa zaidi uhusiano kati ya nchi mbili hizi.
Augustine Mahiga Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwasili asubuhi ya leo hapa mjini Tehran akiuongoza ujumbe wa nchi yake kwa ajili ya kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Iran.