Iran yalaani mashambulio ya kigaidi ndani ya misikiti nchini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i35846-iran_yalaani_mashambulio_ya_kigaidi_ndani_ya_misikiti_nchini_afghanistan
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani mashambulio ya kigaidi yaliyolenga misikiti miwili katika miji ya Kabul na Ghor nchini Afghanistan hapo jana na kusababisha kuuawa na kujeruhiwa makumi ya waumini waliokuwemo ndani ya misikiti hiyo.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Oct 21, 2017 04:16 UTC
  • Iran yalaani mashambulio ya kigaidi ndani ya misikiti nchini Afghanistan

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani mashambulio ya kigaidi yaliyolenga misikiti miwili katika miji ya Kabul na Ghor nchini Afghanistan hapo jana na kusababisha kuuawa na kujeruhiwa makumi ya waumini waliokuwemo ndani ya misikiti hiyo.

Katika radiamali na tamko alilotoa jana hiyohiyo kuhusiana na mashambulio hayo makubwa ya umwagaji damu, Bahram Qassemi mbali na kueleza masikitiko yake na kutoa mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Afghanistan amesema, magaidi wenye kiu ya damu na wakufurishaji majahili ambao hawaijui hata harufu ya dini na utu, kwa mara nyengine tena wamewaandama kwa mashambulio yao yanayotokana na chuki wananchi madhulumu, wanaoteseka na wasio na hatia wa Afghanistan, lengo lao likiwa ni kuzusha hitilafu za kimadhehebu na kuvuruga amani katika nchi jirani ya Afghanistan.

Hali baada ya mripuko wa bomu ndani ya msikiti hapo jana

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu Iran itaendelea kuwa bega kwa bega na serikali na wananchi wanamuqawama wa Afghanistan hadi kuhakikisha mizizi ya machafuko, jinai, ugaidi na ukosefu wa amani imeng'olewa kikamilifu nchini humo.

Watu wasiopungua 72 wakiwemo wanawake na watoto waliuawa hapo jana na makumi ya wengine walijeruhiwa katika mashambulio ya kigaidi yaliyolenga misikiti miwili katika miji ya Kabul na Ghor nchini Afghanistan. Kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) limejigamba na kutangaza kuwa ndilo lililohusika na jinai hiyo.../